3 Alikuwako pamoja naye, amefichwa nyumbani mwa BWANA, miaka sita. Naye Athalia akaitawala nchi.
4 Hata mwaka wa saba Yehoyada akatuma, na kuwaleta wakuu wa mamia, wa Wakari, na wa walinzi, akawaleta kwake ndani ya nyumba ya BWANA; akapatana nao, akawaapisha nyumbani mwa BWANA, akawaonyesha huyo mwana wa mfalme.
5 Akawaamuru, akasema, Hili ndilo neno mtakalolifanya; theluthi yenu, mtakaoingia siku ya sabato, mtayalinda malinzi ya nyumba ya mfalme;
6 na theluthi mtakuwapo mlangoni pa Suri; na theluthi langoni nyuma ya walinzi; hivyo mtayalinda malinzi ya nyumba, kuzuia watu wasiingie.
7 Na sehemu mbili zenu, yaani, wote watokao siku ya sabato, mtayalinda malinzi ya nyumba ya BWANA kumzunguka mfalme.
8 Mtamzunguka mfalme pande zote, kila mtu mwenye silaha zake mkononi; naye awaye yote aingiaye ndani ya safu auawe; mkafuatane na mfalme, akitoka na akiingia.
9 Nao wakuu wa mamia wakafanya sawasawa na yote aliyowaamuru Yehoyada kuhani; wakawatwaa kila mtu watu wake, hao watakaoingia sabato, nao watakaotoka sabato, wakaja kwa Yehoyada kuhani.