19 Wakafanya fitina juu yake katika Yerusalemu, naye akakimbia mpaka Lakishi, lakini wakatuma watu kumfuata mpaka Lakishi, wakamwua huko.
20 Wakamleta juu ya farasi; naye akazikwa huko Yerusalemu pamoja na babaze katika mji wa Daudi.
21 Na watu wote wa Yuda wakamtwaa Uzia, aliyekuwa mwenye umri wa miaka kumi na sita, wakamfanya awe mfalme mahali pa baba yake Amazia.
22 Huyo akajenga Elathi, akaurudisha kwa Yuda, baada ya kulala mfalme pamoja na babaze.
23 Katika mwaka wa kumi na tano wa Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda Yeroboamu mwana wa Yehoashi mfalme wa Israeli alianza kutawala katika Samaria; akatawala miaka arobaini na mmoja.
24 Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA; wala hakuyaacha makosa yote ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli.
25 Yeye akaurudisha mpaka wa Israeli toka kuingia kwa Hamathi hata bahari ya Araba, sawasawa na neno la BWANA, Mungu wa Israeli, alilolinena kwa mkono wa mtumishi wake Yona mwana wa Amitai, nabii, aliyekuwa wa Gath-heferi.