8 Katika mwaka wa thelathini na nane wa Uzia mfalme wa Yuda Zekaria mwana wa Yeroboamu akatawala juu ya Israeli katika Samaria miezi sita.
9 Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA kama walivyofanya babaze; hakuyaacha makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli.
10 Na Shalumu mwana wa Yabeshi akafanya fitina juu yake, akampiga mbele ya watu, akamwua, akatawala mahali pake.
11 Basi mambo yote ya Zekaria yaliyosalia, tazama, yameandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli.
12 Hilo ndilo neno la BWANA alilomwambia Yehu, akisema, Wana wako watakaa kitini mwa Israeli hata kizazi cha nne. Ikawa vivyo hivyo.
13 Huyo Shalumu mwana wa Yabeshi alianza kutawala katika mwaka wa thelathini na kenda wa Uzia mfalme wa Yuda; akatawala muda wa mwezi mmoja katika Samaria.
14 Menahemu mwana wa Gadi akapanda kutoka Tirza, akaja Samaria, akampiga Shalumu mwana wa Yabeshi huko Samaria, akamwua, akatawala mahali pake.