1 Siku hizo Hezekia akaugua, akawa katika hatari ya kufa. Isaya, nabii, mwana wa Amozi, akamjia akamwambia, BWANA asema hivi, Tengeza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona.
2 Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba BWANA akasema,
3 Nakusihi, BWANA, ukumbuke sasa, jinsi nilivyokwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana.
4 Ikawa, kabla Isaya hajatoka katika mji wa kati, neno la BWANA likamjia, kusema,
5 Rudi, ukamwambie Hezekia, mkuu wa watu wangu, BWANA, Mungu wa Daudi baba yako asema hivi, Nimeyasikia maombi yako, na kuyaona machozi yako; tazama, nitakuponya; siku ya tatu utapanda nyumbani kwa BWANA.