1 Yosia alikuwa na umri wa miaka minane alipoanza kutawala; akatawala miaka thelathini na mmoja katika Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Yedida, binti Adaya wa Bozkathi.
2 Akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA, akaenda katika njia yote ya Daudi baba yake, wala hakugeuka upande wa kuume wala wa kushoto.
3 Ikawa, katika mwaka wa kumi na nane wa mfalme Yosia, mfalme akamtuma Shafani, mwana wa Azalia, mwana wa Meshulamu, mwandishi, nyumbani kwa Bwana, akisema,
4 Enenda kwa Hilkia, kuhani mkuu, ili aihesabu fedha yote inayoletwa nyumbani mwa BWANA, ambayo mabawabu wameipokea kwa watu;
5 tena waitie ile fedha katika mikono ya wafanya kazi wanaoisimamia nyumba ya BWANA; wakapewe wafanya kazi waliomo ndani ya nyumba ya BWANA, ili wapate kupatengeneza mahali palipobomoka ndani ya nyumba;
6 wapewe maseremala, na wajenzi, na waashi; ili kununua miti na mawe yaliyochongwa wapate kuitengeneza nyumba.
7 Lakini hawakuulizwa habari za ile fedha waliyokabidhiwa; maana walitenda kazi kwa uaminifu.