8 Naye Hilkia, kuhani mkuu, akamwambia Shafani, mwandishi, Nimekiona kitabu cha torati katika nyumba ya BWANA. Hilkia akampa Shafani kile kitabu, naye akakisoma.
9 Shafani mwandishi akamwendea mfalme, akamletea mfalme habari tena, akasema, Watumishi wako wamezitoa zile fedha zilizoonekana ndani ya nyumba, nao wamewakabidhi wafanya kazi wanaoisimamia nyumba ya BWANA.
10 Kisha Shafani mwandishi akamwambia mfalme, akasema, Hilkia kuhani amenipa kitabu. Shafani akakisoma mbele ya mfalme.
11 Ikawa, mfalme alipokwisha kuyasikia maneno ya kitabu hicho cha torati, alirarua nguo zake.
12 Mfalme akamwamuru Hilkia kuhani, na Ahikamu, mwana wa Shafani, na Akbori, mwana wa Mikaya, na Shafani mwandishi, na Asaya, mtumishi wa mfalme akasema,
13 Enendeni, mkamwulize BWANA kwa ajili yangu, na kwa ajili ya watu hawa, na kwa ajili ya Yuda yote, katika habari za maneno ya kitabu hiki kilichoonekana; kwa kuwa hasira ya BWANA ni kubwa aliyotukasirikia, kwa sababu baba zetu hawakuyaangalia maneno ya kitabu hiki, kufanya kama hayo yote tuliyoandikiwa.
14 Basi Hilkia kuhani, na Ahikamu, na Akbori, na Shafani, na Asaya, wakamwendea Hulda, nabii mke, mkewe Shalumu, mwana wa Tikva, mwana wa Harhasi, mtunza mavazi ya mfalme; (naye alikaa Yerusalemu katika mtaa wa pili;) wakasema naye.