18 Akasema, Mwacheni; mtu awaye yote asiiondoe mifupa yake. Basi wakaiacha mifupa yake, pamoja na mifupa ya yule nabii aliyetoka Samaria.
19 Na nyumba zote pia za mahali pa juu palipokuwa katika miji ya Samaria, wafalme wa Israeli walizozifanya, ili kumkasirisha BWANA, Yosia aliziondoa, akazitenda kwa mfano wa mambo yote aliyoyatenda katika Betheli.
20 Akawaua na makuhani wote wa mahali pa juu waliokuwako huko, juu ya madhabahu, akateketeza mifupa ya watu juu yake; kisha akarejea Yerusalemu.
21 Naye mfalme akawaamuru watu wote, akasema, Mfanyieni BWANA, Mungu wenu, pasaka, kama ilivyoandikwa katika kitabu hiki cha agano.
22 Hakika yake haikufanyika pasaka kama hiyo, tangu zamani za waamuzi waliowaamua Israeli, wala katika zamani za wafalme wa Israeli, wala za wafalme wa Yuda.
23 Bali katika mwaka wa kumi na nane wa mfalme Yosia ilifanyika pasaka hii kwa BWANA ndani ya Yerusalemu.
24 Tena wenye pepo wa utambuzi, na wachawi, na vinyago, na sanamu, na machukizo yote yaliyoonekana katika nchi ya Yuda na katika Yerusalemu, Yosia akayaondoa yote, ili apate kuyathibitisha maneno ya torati yaliyoandikwa katika kile kitabu alichokiona Hilkia kuhani ndani ya nyumba ya BWANA.