21 Naye mfalme akawaamuru watu wote, akasema, Mfanyieni BWANA, Mungu wenu, pasaka, kama ilivyoandikwa katika kitabu hiki cha agano.
22 Hakika yake haikufanyika pasaka kama hiyo, tangu zamani za waamuzi waliowaamua Israeli, wala katika zamani za wafalme wa Israeli, wala za wafalme wa Yuda.
23 Bali katika mwaka wa kumi na nane wa mfalme Yosia ilifanyika pasaka hii kwa BWANA ndani ya Yerusalemu.
24 Tena wenye pepo wa utambuzi, na wachawi, na vinyago, na sanamu, na machukizo yote yaliyoonekana katika nchi ya Yuda na katika Yerusalemu, Yosia akayaondoa yote, ili apate kuyathibitisha maneno ya torati yaliyoandikwa katika kile kitabu alichokiona Hilkia kuhani ndani ya nyumba ya BWANA.
25 Kabla ya huyo hapakuwa na mfalme mfano wake, aliyemwelekea BWANA kwa moyo wake wote, na kwa roho yake yote, na kwa nguvu zake zote, sawasawa na sheria zote za Musa; wala baada yake hakuinuka mmoja mfano wake yeye.
26 Walakini BWANA hakuuacha ukali wa ghadhabu yake nyingi, ambayo kwayo hasira yake iliwaka juu ya Yuda, kwa sababu ya machukizo yote ambayo Manase amemchukiza.
27 BWANA akasema Nitawahamisha Yuda pia mbali nami, kama nilivyowahamisha Israeli, nami nitautupa mji huu niliouchagua, naam, Yerusalemu, na nyumba ile niliyoinena, Jina langu litakuwa humo.