6 Naye akaiondoa Ashera katika nyumba ya BWANA, nje ya Yerusalemu, mpaka Kidroni, akaipiga moto penye kijito cha Kidroni, na kuiponda-ponda iwe mavumbi, akayatupa mavumbi yake juu ya makaburi ya watu.
7 Akaziangusha nyumba za mahanithi, waliokuwamo nyumbani mwa BWANA, wanawake walipofuma mapazia ya Ashera.
8 Akawatoa makuhani wote katika miji ya Yuda, akapanajisi mahali pa juu, makuhani walipokuwa wamefukiza uvumba, tangu Geba hata Beer-sheba; akapavunja mahali pa juu pa malango, palipokuwapo penye kuingia lango la Yoshua, liwali wa mji, palipokuwa upande wa kushoto wa mtu langoni pa mji.
9 Walakini hao makuhani wa mahali pa juu hawakupanda madhabahuni kwa BWANA katika Yerusalemu, bali wakala mikate isiyo na chachu katikati ya ndugu zao.
10 Naye akainajisi Tofethi, iliyomo katika bonde la wana wa Hinomu, ili mtu asipitishe mwana wake au binti yake motoni kwa Moleki.
11 Akawaondoa farasi ambao wafalme wa Yuda waliwatoa kwa jua, hapo pa kuingia nyumbani mwa BWANA, karibu na chumba cha Nathan-Meleki, towashi, kilichohuwako kiungani; akayapiga moto magari ya jua.
12 Nazo madhabahu zilizokuwako darini juu ya chumba cha juu cha Ahazi, wafalme wa Yuda walizozifanya, nazo madhabahu alizozifanya Manase katika behewa mbili za nyumba ya BWANA, mfalme akazivunja, akazitelemsha huko nje, na kuyatupa mavumbi yake katika kijito cha Kidroni.