14 Elisha akasema, Kama BWANA wa majeshi aishivyo, ambaye nimesimama mbele zake, kama singemwangalia uso wake Yehoshafati mfalme wa Yuda, singekutazama, wala kuonana nawe.
15 Ila sasa niletee mpiga kinanda. Ikawa, mpiga kinanda alipokipiga, mkono wa BWANA ukamjia juu yake.
16 Akasema, BWANA asema hivi, Fanyeni bonde hili lijae mahandaki.
17 Kwa kuwa BWANA asema hivi, Hamutauona upepo, wala hamtaiona mvua, ila bonde hilo litajaa maji; nanyi mtakunywa, ninyi, na ng’ombe zenu, na wanyama wenu.
18 Na jambo hili ni jepesi machoni pa BWANA; pia atawatia Wamoabi mikononi mwenu.
19 Nanyi mtapiga kila mji wenye boma, na kila mji ulio mzuri, na kila mti mwema mtaukata, na chemchemi zote za maji mtaziziba, na kila mahali palipo pema mtapaharibu kwa mawe.
20 Ikawa asubuhi, wakati wa kutoa sadaka ya unga, tazama, maji yakaja kwa njia ya Edomu, hata nchi ikajaa maji.