5 Lakini ikawa, Ahabu alipokufa, mfalme wa Moabu akamwasi mfalme wa Israeli.
6 Akatoka wakati ule ule mfalme Yoramu katika Samaria, akawahesabu Israeli wote.
7 Akaenda akatuma kwa Yehoshafati mfalme wa Yuda, akasema, Mfalme wa Moabu ameniasi; je! Utakwenda pamoja nami tupigane na Moabu? Akasema, Nitakwenda; mimi ni kama wewe, watu wangu ni kama watu wako, farasi zangu ni kama farasi zako.
8 Akauliza, Njia ipi tuiendee? Akajibu, Njia ya jangwa la Edomu.
9 Basi mfalme wa Israeli akaenda, na mfalme wa Yuda, na mfalme wa Edomu; wakazunguka mwendo wa siku saba; wala hapakuwa na maji kwa jeshi, wala kwa wanyama waliowafuata.
10 Mfalme wa Israeli akasema, Ole wetu! Kwani BWANA amewakutanisha hawa wafalme watatu, awaue mkononi mwa Moabu.
11 Lakini Yehoshafati akasema, Je! Hapana hapa nabii wa BWANA, ili tumwulize BWANA kwa yeye? Akajibu mtumishi mmoja wa mfalme wa Israeli, akasema, Yupo hapa Elisha mwana wa Shafati, aliyekuwa akimimina maji juu ya mikono yake Eliya.