1 Basi Naamani, jemadari wa jeshi la mfalme wa Shamu, alikuwa mtu mkubwa mbele ya bwana wake, na mwenye kuheshimiwa, kwa sababu kwa mkono wake BWANA alikuwa amewapa Washami kushinda; tena alikuwa mtu hodari wa vita; lakini alikuwa mwenye ukoma.
2 Na Washami walikuwa wametoka vikosi, wakachukua mfungwa mmoja kijana mwanamke kutoka nchi ya Israeli; naye akamhudumia mkewe Naamani.
3 Akamwambia bibi yake, Laiti bwana wangu angekuwa pamoja na yule nabii aliyeko Samaria! Maana angemponya ukoma wake.
4 Mtu mmoja akaingia, akamwambia bwana wake, akasema, Yule kijana mwanamke aliyetoka nchi ya Israeli asema hivi na hivi.
5 Mfalme wa Shamu akasema, Haya! Basi, mimi nitampelekea mfalme wa Israeli waraka. Basi akaenda zake, akachukua mikononi mwake talanta kumi za fedha, na vipande vya dhahabu elfu sita, na mavazi kumi.
6 Akampelekea mfalme wa Israeli waraka ule, kusema, Waraka huu utakapokuwasilia, tazama, nimemtuma mtumishi wangu Naamani kwako, ili upate kumponya ukoma wake.