6 Lakini Yeroboamu mwana wa Nebati, mtumwa wa Sulemani mwana wa Daudi, akainuka, akamfanyia fitina bwana wake.
7 Wakamkusanyikia watu mabaradhuli, wasiofaa kitu, waliojitia nguvu juu ya Rehoboamu mwana wa Sulemani, Rehoboamu alipokuwa kijana na wa moyo mwororo, asiweze kuwazuia.
8 Hata sasa mwajidhania kuwa mtauzuia ufalme wa BWANA mikononi mwa wana wa Daudi; nanyi mmekuwa jamii kubwa, na kwenu mna ndama za dhahabu alizowafanyia Yeroboamu kuwa miungu.
9 Je! Hamkuwafukuza makuhani wa BWANA, wana wa Haruni, na Walawi; mkajifanyia makuhani kama wafanyavyo watu wa nchi nyingine? Hata ye yote ajaye kujifanya wakfu na ndama, na kondoo waume saba, aweza kuwa kuhani wa hiyo isiyo miungu.
10 Lakini sisi, BWANA ndiye Mungu wetu, wala sisi hatukumwacha; tena tunao makuhani wanaomtumikia BWANA, wana wa Haruni, na Walawi, kwa kazi yao;
11 nao humtolea BWANA kila asubuhi, na kila jioni, sadaka za kuteketezwa na fukizo la manukato; mikate ya wonyesho pia huiweka kwa taratibu yake juu ya meza takatifu, na kinara cha dhahabu chenye taa zake, kuwaka kila jioni; kwa maana sisi twayalinda malinzi ya BWANA, Mungu wetu; bali ninyi mmemwacha.
12 Na tazama, Mungu yu pamoja nasi atutangulie, na makuhani wake wenye mapanda, ili wapige sauti ya kugutusha juu yenu. Enyi wana wa Israeli, msipigane na BWANA, Mungu wa baba zenu; kwani hamtafanikiwa.