1 Yehoshafati mfalme wa Yuda akarudi Yerusalemu nyumbani kwake kwa amani.
2 Yehu mwana wa Hanani mwonaji akatoka kwenda kumlaki, akamwambia mfalme Yehoshafati, Je! Imekupasa kuwasaidia waovu, na kuwapenda wamchukiao BWANA? Kwa ajili ya hayo ghadhabu i juu yako itokayo kwa BWANA.
3 Walakini yameonekana mema ndani yako, kwa kuwa umeyaondoa maashera katika nchi, na moyo wako umeukaza kumtafuta Mungu.
4 Na Yehoshafati akakaa Yerusalemu; akatoka tena kwenda kati ya watu toka Beer-sheba mpaka milima ya Efraimu, akawarudisha kwa BWANA, Mungu wa baba zao.