4 Na Yehoshafati akakaa Yerusalemu; akatoka tena kwenda kati ya watu toka Beer-sheba mpaka milima ya Efraimu, akawarudisha kwa BWANA, Mungu wa baba zao.
5 Akasimamisha makadhi katika nchi, katikati ya miji yote yenye maboma ya Yuda, mji kwa mji;
6 akawaambia hao makadhi, Angalieni myafanyayo; kwa kuwa hammfanyii mwanadamu hukumu, ila BWANA; naye yupo pamoja nanyi katika neno la hukumu.
7 Basi sasa hofu ya BWANA na iwe juu yenu; angalieni mkaifanye; kwa maana kwa BWANA, Mungu wetu, hapana uovu, wala kujali nafsi za watu, wala kupokea zawadi.
8 Tena katika Yerusalemu Yehoshafati akasimamisha wa Walawi na makuhani, na wakuu wa mbari za mababa wa Israeli wawe kwa hukumu ya BWANA, na kwa mateto. Nao wakarudi Yerusalemu.
9 Akawaagiza, akasema, Ndivyo mtakavyotenda kwa hofu ya BWANA, kwa uaminifu, na kwa moyo kamili.
10 Na kila mara watakapowajia na teto ndugu zenu wakaao mijini mwao, kati ya damu na damu, kati ya torati na amri, sheria na hukumu, mtawaonya, wasiingie hatiani mbele za BWANA, mkajiliwa na ghadhabu ninyi na ndugu zenu; fanyeni haya wala hamtakuwa na hatia.