1 Basi Sulemani alikusudia kujenga nyumba kwa jina la BWANA, na kuujengea ufalme wake nyumba.
2 Sulemani akahesabu watu sabini elfu wawe wachukuzi wa mizigo, na watu themanini elfu wawe wachongaji milimani, na elfu tatu na mia sita wawe wasimamizi wao.
3 Sulemani akatuma watu kwa Hiramu mfalme wa Tiro, akisema, Kama ulivyomtendea baba yangu Daudi, na kumletea mierezi, ajijengee nyumba ya kukaa, unitendee na mimi.
4 Angalia, najenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wangu, ili kumfanyia wakfu, ya kufukizia mbele zake fukizo la manukato, na ya mkate wa wonyesho wa daima, na ya sadaka za kuteketezwa za asubuhi na jioni, na za siku za sabato, na za mwezi mpya, na za sikukuu zilizoagizwa za BWANA, Mungu wetu. Hili ni agizo la milele kwa Israeli.
5 Nayo nyumba nitakayoijenga ni kubwa; kwa sababu Mungu wetu ndiye mkuu juu ya miungu yote.
6 Lakini ni nani awezaye kumjengea nyumba, ikiwa mbingu hazimtoshi, wala mbingu za mbingu? Nami ni nani basi, hata nimjengee nyumba, isipokuwa kwa ajili ya kufukizia fukizo mbele zake?
7 Unipelekee basi mtu mstadi wa kazi ya dhahabu, na ya fedha, na ya shaba, na ya chuma, na ya urujuani, na nyekundu, na samawi, mwenye kujua kuchora machoro, pamoja na wastadi walioko Yuda na Yerusalemu pamoja nami, aliowaweka baba yangu Daudi.