8 Na Waamoni wakampa Uzia zawadi; likaenea jina lake mpaka pa kuingilia Misri; kwa kuwa akaongezeka nguvu mno.
9 Tena Uzia akaujengea Yerusalemu minara, penye lango la pembeni, na penye lango la bonde, na ugeukapo ukuta, akaitia nguvu.
10 Akajenga minara tena nyikani, akachimba mabirika mengi, maana alikuwa na ng’ombe tele; katika Shefela pia, na katika nchi tambarare; tena alikuwa na wakulima na watunza mizabibu milimani, na katika mashamba ya neema; maana yeye alipenda ukulima.
11 Zaidi ya hayo Uzia alikuwa na jeshi la watu wa kupigana, waliokwenda vitani vikosi vikosi, sawasawa na hesabu walivyohesabiwa na Yeieli mwandishi, na Maaseya msimamizi, chini ya mkono wa Hanania, mmojawapo wa maakida wa mfalme.
12 Hesabu yote ya wakuu wa nyumba za mababa, watu mashujaa, ilikuwa elfu mbili na mia sita.
13 Na chini ya mkono wao kulikuwa na jeshi la askari, mia tatu na saba elfu, na mia tano, ambao walipigana vita kwa nguvu nyingi, kumsaidia mfalme juu ya adui.
14 Uzia akawafanyizia jeshi lote ngao na mikuki, na chapeo, na deraya za madini, na nyuta, na mawe ya kupiga kwa teo.