2 Basi Hezekia, alipoona ya kuwa Senakeribu amekuja, na kuazimia kupigana na Yerusalemu,
3 akafanya shauri na wakuu wake, na mashujaa wake, kuzuia maji ya chemchemi zilizokuwa nje ya mji; nao wakamsaidia.
4 Wakakusanyika watu wengi, wakazizuia chemchemi zote, na kijito kilichopita kati ya nchi, wakisema, Kwa nini, wakifika wafalme wa Ashuru, waone maji mengi?
5 Akapiga moyo konde, akaujenga ukuta wote uliobomoka, akauinua sawa na minara, na ukuta wa pili nje, akaongeza nguvu ya Milo, katika mji wa Daudi, akafanya silaha na ngao tele.
6 Akaweka maakida wa vita juu ya watu, akawakusanya kwake uwandani penye lango la mji, akawafurahisha mioyo; akisema,
7 Iweni hodari, na wa moyo mkuu, msiogope, wala msifadhaike kwa sababu ya mfalme wa Ashuru, wala kwa majeshi yote walio pamoja naye; kwa maana yupo mkuu pamoja nasi kuliko aliye pamoja naye;
8 kwake upo mkono wa mwili; ila kwetu yupo BWANA, Mungu wetu, kutusaidia, na kutupigania mapigano yetu. Na watu wakayategemea maneno ya Hezekia, mfalme wa Yuda.