1 Manase alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka hamsini na mitano.
2 Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, sawasawa na machukizo yote ya mataifa, aliowafukuza BWANA mbele ya wana wa Israeli.
3 Kwa maana akapajenga tena mahali pa juu alipopabomoa Hezekia babaye; akazisimamisha madhabahu za mabaali, akafanya na sanamu za maashera, akaabudu jeshi lote la mbinguni, na kulitumikia.
4 Akajenga madhabahu katika nyumba ya BWANA, napo ndipo alipopanena BWANA, Katika Yerusalemu litakuwako jina langu milele.
5 Akajenga madhabahu kwa ajili ya jeshi lote la mbinguni katika nyua mbili za nyumba ya BWANA.
6 Tena akawapitisha wanawe motoni katika bonde la mwana wa Hinomu; akatazama bao, akabashiri, akafanya uganga, akajishughulisha na hao wenye pepo wa utambuzi, na wachawi; akafanya mabaya mengi machoni pa BWANA, hata kumkasirisha.