1 Yosia alikuwa na umri wa miaka minane alipoanza kutawala; akatawala miaka thelathini na mmoja huko Yerusalemu.
2 Akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA, akaziendea njia za Daudi babaye, asigeuke kwa kuume wala kwa kushoto.
3 Kwa kuwa katika mwaka wa nane wa kutawala kwake, naye akali mchanga, alianza kumtafuta Mungu wa Daudi babaye; hata katika mwaka wa kumi na mbili akaanza kusafisha Yuda na Yerusalemu kwa kuondoa mahali pa juu, na kwa kuondoa maashera, na sanamu za kuchora, nazo za kusubu.
4 Wakazibomoa madhabahu za mabaali machoni pake; na sanamu za jua, zilizoinuliwa juu yake, akazikata-kata; na maashera, na sanamu za kuchonga, nazo za kusubu, akazivunja-vunja, akaziponda kuwa mavumbi, akayamimina juu ya makaburi ya hao waliozichinjia dhabihu.
5 Akaiteketeza mifupa ya makuhani madhabahuni mwao, akasafisha Yuda na Yerusalemu.
6 Na katika miji ya Manase, na Efraimu, na Simeoni, mpaka Naftali, akafanya vile vile; na katika maganjo yake pande zote.
7 Akazibomoa madhabahu, akaponda-ponda maashera na sanamu kuwa mavumbi, akazikata-kata sanamu zote za jua katika nchi yote ya Israeli, kisha akarejea Yerusalemu.