3 Akawaambia Walawi, waliowafundisha Israeli wote, waliotakasika kwa BWANA, Wekeni sanduku takatifu katika nyumba aliyoijenga Sulemani, mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli; hamtakuwa tena na mzigo mabegani; sasa mtumikieni BWANA, Mungu wenu, na watu wake Israeli.
4 Mkajiweke tayari kwa kadiri ya nyumba za baba zenu, kwa zamu zenu, kama alivyoandika Daudi mfalme wa Israeli, na kama alivyoandika Sulemani mwanawe.
5 Mkasimame katika patakatifu, kama walivyogawanyika ndugu zenu, wana wa watu, kufuata nyumba za mababa, kadiri ya mgawanyiko wa kila nyumba ya baba, ya Walawi.
6 Mkachinje pasaka, mkajitakase, mkawatengenezee ndugu zenu, kutenda sawasawa na neno la BWANA kwa mkono wa Musa.
7 Tena Yosia akawapa wana wa watu, matoleo ya makundi, wana-kondoo na wana-mbuzi, yote yawe kwa ajili ya matoleo ya pasaka, wote waliokuwako, wakipata thelathini elfu, na ng’ombe elfu tatu; hao walitoka katika mali za mfalme.
8 Na wakuu wake wakawapa watu, na makuhani na Walawi matoleo ya hiari. Hilkia na wana na Yehieli, wakubwa wa nyumba ya Mungu, wakawapa makuhani, kuwa matoleo ya pasaka, wana-kondoo elfu mbili na mia sita, na ng’ombe mia tatu.
9 Konania naye, na Shemaya, na Nethaneli, ndugu zake, na Hashabia, na Yeieli, na Yozabadi, wakuu wa Walawi, wakawapa Walawi, kuwa matoleo ya pasaka, wana-kondoo elfu tano, na ng’ombe mia tano.