17 Mfalme akatoka, na watu wote wakamfuata; wakakaa kidogo katika Beth-merhaki.
18 Watumishi wake wote wakapita karibu naye; na Wakerethi wote, na Wapelethi wote, na Wagiti wote, watu mia sita walioandamana naye kutoka Gathi, wakapita mbele ya mfalme.
19 Ndipo mfalme akamwambia Itai, Mgiti, Mbona wewe unakwenda pamoja nasi? Rudi, ukakae na mfalme; maana wewe u mgeni, tena u mtu uliyefukuzwa mahali pako mwenyewe.
20 Kwa kuwa umekuja jana tu kwa nini nikusumbue leo, na kukuzungusha huko na huko pamoja nasi nami hapa naenda niwezapo kwenda? Rudi wewe, ukawarudishe na ndugu zako; rehema na kweli ziwe pamoja nawe.
21 Naye Itai akamjibu mfalme akasema, Kama aishivyo BWANA, na bwana wangu mfalme aishivyo, hakika yake kila mahali atakapokuwapo mfalme, bwana wangu, ikiwa ni kwa kufa au ikiwa ni kwa kuishi, ndipo atakapokuwapo na mtumwa wako.
22 Basi Daudi akamwambia Itai, Haya, enenda ukavuke. Akavuka Itai, Mgiti na watu wake wote, na watoto wadogo wote waliokuwa pamoja naye.
23 Na nchi yote ikalia kwa sauti kuu, nao watu wote wakavuka, mfalme mwenyewe naye akavuka kile kijito Kidroni, na hao watu wote wakavuka, wakielekea njia ya nyika.