30 Daudi akapanda akishika njia ya kuupandia mlima wa Mizeituni, akilia alipokuwa akipanda; naye alikuwa amejifunika kichwa chake, akaenda hana viatu; na watu wote waliokuwa pamoja naye wakajifunika vichwa vyao, kila mmoja wao, wakapanda juu, wakilia walipopanda.
31 Mtu mmoja akamwambia Daudi ya kwamba, Ahithofeli yu katika hao waliopatana na Absalomu; Daudi akasema, Ee BWANA, nakusihi, uligeuze shauri la Ahithofeli liwe ubatili.
32 Ikawa, Daudi alipofika juu, hapo Mungu alipoabudiwa, tazama, Hushai, Mwarki, akaja kumlaki na joho lake limeraruliwa, tena ana udongo kichwani mwake.
33 Daudi akamwambia, Ukienda mbele pamoja nami, utakuwa mzigo kwangu;
34 lakini ukirudi mjini, na kumwambia Absalomu, Nitakuwa mtumishi wako, Ee mfalme; kama vile nilivyokuwa mtumishi wa baba yako tokea zamani, ndivyo nitakavyokuwa mtumishi wako sasa; ndipo utayavunja mashauri ya Ahithofeli kwa ajili yangu.
35 Je! Hawako Sadoki na Abiathari, makuhani, pamoja nawe huko? Basi itakuwa, kila neno utakalolisikia katika jumba la mfalme, utawaambia Sadoki na Abiathari, makuhani.
36 Angalia, wanao huko pamoja nao wana wao wawili, Ahimaasi, mwana wa Sadoki, na Yonathani, mwana wa Abiathari; nanyi kwa mikono yao mtanipelekea habari ya kila neno mtakalolisikia.