13 naye akaileta toka huko hiyo mifupa ya Sauli, na mifupa ya Yonathani mwanawe; nao wakaizoa mifupa yao waliotundikwa.
14 Kisha wakaizika mifupa ya Sauli na ya Yonathani mwanawe katika nchi ya Benyamini, huko Zela, kaburini mwa Kishi babaye; wakafanya yote aliyoyaamuru mfalme. Na baadaye Mungu aliiridhia hiyo nchi.
15 Basi kulikuwa na vita tena kati ya Wafilisti na Israeli; Daudi akashuka mpaka Gobu, na watumishi wake pamoja naye, akapigana na Wafilisti; naye Daudi akaishiwa na nguvu.
16 Naye Ishi-benobu, aliyekuwa mmojawapo wa Warefai, ambaye uzito wa mkuki wake ulikuwa shekeli mia tatu za shaba kwa uzani, naye amejifungia upanga mpya, alijaribu kumwua Daudi.
17 Lakini Abishai, mwana wa Seruya, akamsaidia, akampiga Mfilisti, akamwua. Ndipo watu wa Daudi wakamwapia, wakasema, Wewe hutatoka tena pamoja nasi kwenda vitani, usije ukaizima taa ya Israeli.
18 Ikawa baada ya hayo, kulikuwa na vita tena na Wafilisti huko Gobu; ndipo Sibekai, Mhushathi, alipomwua Safu, aliyekuwa mmojawapo wa Warefai.
19 Kulikuwa na vita tena na Wafilisti huko Gobu; na Elhanani, mwana wa Yairi, Mbethlehemi, alimwua Goliathi, Mgiti, ambaye mti wa mkuki wake ulikuwa kama mti wa mfumaji.