2 Ndipo mfalme akawaita Wagibeoni akawaambia; (basi Wagibeoni si wa wana wa Israeli, ila ni wa masalio ya Waamori; na wana wa Israeli walikuwa wamewaapia; lakini Sauli akatafuta kuwaua katika juhudi yake kwa ajili ya wana wa Israeli na Yuda;)
3 basi Daudi akawaambia hao Wagibeoni, Niwatendee nini? Na kwa tendo gani nifanye upatanisho, mpate kuubariki urithi wa BWANA?
4 Na hao Wagibeoni wakamwambia, Si jambo la fedha wala dhahabu lililo kati ya sisi na Sauli, au nyumba yake; wala si juu yetu kumwua mtu ye yote katika Israeli. Akasema Mtakayoyanena, ndiyo nitakayowatendea ninyi.
5 Wakamwambia mfalme, Yule mtu aliyetupoteza, na kutufanyia shauri la kutuharibu, tusikae katika mipaka yo yote ya Israeli,
6 basi, na tutolewe watu saba katika wanawe, nasi tutawatundika mbele za BWANA katika Gibeoni, katika mlima wa BWANA. Mfalme akasema, Nitawatoa.
7 Lakini mfalme akamwachilia Mefiboshethi, mwana wa Yonathani, mwana wa Sauli, kwa ajili ya kiapo cha BWANA kilichokuwa kati yao, yaani, kati ya Daudi na Yonathani, mwana wa Sauli.
8 Ila mfalme akawatwaa hao wana wawili wa Rispa, binti Aya, aliomzalia Sauli, Armoni na Mefiboshethi; na wana watano wa Merabu binti Sauli, aliomzalia Adrieli, mwana wa Barzilai, Mmeholathi;