16 Basi hao mashujaa watatu wakapenya jeshi la Wafilisti, wakateka maji kutoka kile kisima cha Bethlehemu, kilicho karibu na lango, wakayachukua, wakamletea Daudi; walakini yeye hakukubali kuyanywa, akayamimina mbele za BWANA.
17 Akasema, Hasha, BWANA, nisifanye hivi; je! Si damu hii ya watu hao waliohatirisha nafsi zao? Kwa hiyo hakukubali kuyanywa. Hayo ndiyo waliyoyafanya wale mashujaa watatu.
18 Tena, Abishai, nduguye Yoabu, mwana wa Seruya, alikuwa mkuu wa wale watatu. Huyo aliuinua mkuki wake juu ya watu mia tatu, akawaua, akawa na jina kati ya wale watatu.
19 Je! Huyo hakuwa na heshima maalumu miongoni mwa wale watatu? Kwa hiyo akawekwa kuwa akida wao; ila hakudiriki kuwamo katika wale watatu.
20 Tena Benaya, mwana wa Yehoyada, mtu hodari wa Kabseeli aliyekuwa amefanya mambo makuu; aliwaua simba wakali wawili wa Moabu, pia akashuka akamwua simba katikati ya shimo wakati wa theluji;
21 huyo naye akamwua Mmisri, mtu mrefu; naye huyo Mmisri alikuwa na mkuki mkononi; lakini yeye alimshukia na gongo, akamnyakulia Mmisri mkuki mkononi mwake, akamwua kwa mkuki wake mwenyewe.
22 Hayo ndiyo aliyoyafanya Benaya, mwana wa Yehoyada, akawa na jina kati ya wale mashujaa watatu.