17 tena ikiwa ameuzuia mkono wake asimwonee maskini, wala hakupokea faida na ziada, naye amezifanya hukumu zangu, na kuzifuata sheria zangu; hatakufa huyu kwa sababu ya uovu wa baba yake, hakika ataishi.
18 Kwa habari za yule baba yake, kwa sababu aliwaonea watu kwa ukali mwingi, na kumnyang’anya ndugu yake mali yake kwa nguvu; na kuyatenda yasiyo mema kati ya watu wake, tazama, atakufa katika uovu wake.
19 Lakini ninyi mwasema, Kwani yule mwana asiuchukue uovu wa baba yake? Yule mwana atakapofanya yaliyo halali na haki, na kuzishika amri zangu na kuzitenda, hakika ataishi.
20 Roho itendayo dhambi, ndiyo itakayokufa; mwana hatauchukua uovu wa baba yake, wala baba hatauchukua uovu wa mwanawe, haki yake mwenye haki itakuwa juu yake, na uovu wake mwenye uovu utakuwa juu yake.
21 Lakini mtu mbaya akighairi, na kuacha dhambi zake zote alizozitenda, na kuzishika amri zangu zote, na kutenda yaliyo halali na haki, hakika ataishi, hatakufa.
22 Dhambi zake zote alizozitenda hazitakumbukwa juu yake hata mojawapo; katika haki yake aliyoitenda ataishi.
23 Je! Mimi ninafurahia kufa kwake mtu mwovu? Asema Bwana MUNGU; si afadhali kwamba aghairi, na kuiacha njia yake, akaishi?