23 Neno la BWANA likanijia, kusema,
24 Mwanadamu, uiambie nchi, Wewe u nchi isiyosafika, wala kunyeshewa mvua siku ya ghadhabu.
25 Fitina ya manabii wake imo ndani yake, kama simba angurumaye akirarua mawindo; wamekula roho za watu; hutwaa kwa nguvu hazina na vitu vya thamani; wameongeza hesabu ya wajane wake ndani yake.
26 Makuhani wake wameihalifu sheria yangu, wametia unajisi vitu vyangu vitakatifu; hawakuweka tofauti ya vitu vitakatifu na vitu vya kutumiwa sikuzote; wala hawakuwafundisha watu kupambanua vitu vichafu na vitu vilivyo safi, nao wamefumba macho yao, wasiziangalie sabato zangu, nami nimetiwa unajisi kati yao.
27 Wakuu wake kati yake wamekuwa kama mbwa-mwitu wakirarua mawindo; ili kumwaga damu, na kuharibu roho za watu, wapate faida kwa njia isiyo halali.
28 Na manabii wake wamewapakia chokaa isiyokorogwa vema, wakiona ubatili, na kuwatabiria maneno ya uongo, wakisema, Bwana MUNGU asema hivi; iwapo BWANA hakusema neno.
29 Watu wa nchi wametumia udhalimu, wamenyang’anya kwa nguvu; naam, wamewatenda jeuri maskini na wahitaji, nao wamewaonea wageni bila haki.