8 Tazama, nimeufanya uso wako kuwa mgumu juu ya nyuso zao, na kipaji cha uso chako kuwa kigumu juu ya vipaji vya nyuso vyao.
9 Kama almasi ilivyo ngumu kuliko gumegume, ndivyo nilivyokifanya kipaji chako; usiwaogope, wala usifadhaike kwa sababu ya nyuso zao, wajapokuwa ni nyumba ya kuasi.
10 Tena akaniambia, Mwanadamu, maneno yangu yote nitakayokuambia, yapokee moyoni mwako, na kuyasikia kwa masikio yako.
11 Haya! Enenda uwafikilie watu hao waliohamishwa, kwa wana wa watu wako, ukaseme nao, na kuwaambia, Bwana MUNGU asema hivi; kwamba watasikia, au kwamba hawataki kusikia.
12 Ndipo roho ikaniinua, nami nikasikia nyuma yangu sauti kama mshindo wa radi kuu, ikisema, Na uhimidiwe utukufu wa BWANA tokea mahali pake.
13 Nikasikia mshindo wa mabawa ya vile viumbe hai, walipogusana, na mshindo wa yale magurudumu kando yao, mshindo wa radi kuu.
14 Basi roho ikaniinua, ikanichukua mahali pengine; nami nikaenda kwa uchungu, na hasira kali rohoni mwangu, na mkono wa BWANA ulikuwa juu yangu kwa nguvu.