28 Nami nitaifanya nchi kuwa ukiwa na ajabu, na kiburi cha uwezo wake kitakoma; nayo milima ya Israeli itakuwa ukiwa, asipite mtu.
29 Ndipo watakapojua ya kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapoifanya nchi kuwa ukiwa na ajabu, kwa sababu ya machukizo yao yote waliyoyatenda.
30 Nawe, mwanadamu, wana wa watu wako husimulia habari zako karibu na kuta, na ndani ya milango ya nyumba zao, na kuambiana, kila mtu na ndugu yake, wakisema, Haya! Twende tukasikie ni neno gani hilo litokalo kwa BWANA.
31 Nao huja kwako kama watu wajavyo, nao hukaa mbele yako kama watu wangu, nao husikia maneno yako, wasiyatende; maana kwa vinywa vyao hujifanya kuwa wenye upendo mwingi, lakini mioyo yao inatafuta faida yao.
32 Na tazama, wewe umekuwa kwao kama wimbo mzuri sana, wa mtu mwenye sauti ipendezayo, awezaye kupiga kinanda vizuri; maana, wasikia maneno yako, lakini hawayatendi.
33 Na hayo yatakapokuwapo (tazama, yanakuja), ndipo watakapojua ya kuwa nabii amekuwapo kati yao.