20 Nawe utatwaa baadhi ya damu yake, na kuitia juu ya pembe zake nne, na juu ya ncha nne za daraja, na juu ya pambizo yake pande zote; ndivyo utakavyoitakasa, na kuifanyia upatanisho.
21 Tena utamtwaa ng’ombe wa sadaka ya dhambi, naye utamteketeza mahali palipoamriwa pa nyumba ile, nje ya mahali patakatifu.
22 Na siku ya pili utamtoa beberu mkamilifu awe sadaka ya dhambi; nao wataisafisha madhabahu, kama walivyoisafisha kwa ng’ombe huyo.
23 Utakapokwisha kuitakasa, utatoa ng’ombe mume mchanga mkamilifu, na kondoo mume wa kundini mkamilifu.
24 Nawe utawaleta karibu mbele za BWANA, na makuhani watamwaga chumvi juu yao, nao watawatoa wawe sadaka za kuteketezwa kwa BWANA.
25 Kwa muda wa siku saba utaweka tayari mbuzi kila siku awe sadaka ya dhambi; pia wataweka tayari ng’ombe mume mchanga, na kondoo mume wa kundini, wakamilifu.
26 Kwa muda wa siku saba wataifanyia madhabahu upatanisho, na kuitakasa; ndivyo watakavyoiweka wakfu.