2 Wakasema, Je! Ni kweli BWANA amenena na Musa tu? Hakunena na sisi pia? BWANA akasikia maneno yao.
3 Basi huyo mtu, huyo Musa, alikuwa mpole sana zaidi ya wanadamu wote waliokuwa juu ya uso wa nchi.
4 BWANA akanena ghafula na Musa, na Haruni na Miriamu, na kuwaambia, Tokeni nje ninyi watatu, mwende hemani mwa kukutania. Basi hao watatu wakatoka nje.
5 BWANA akashuka katika nguzo ya wingu akasimama pale mlangoni pa Hema, akawaita Haruni na Miriamu, nao wakatoka nje wote wawili.
6 Kisha akawaambia,Sikizeni basi maneno yangu;Akiwapo nabii kati yenu,Mimi, BWANA, nitajifunua kwake katika maono,Nitasema naye katika ndoto.
7 Sivyo ilivyo kwa mtumishi wangu, Musa;Yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote;
8 Kwake nitanena mdomo kwa mdomo,Maana, waziwazi wala si kwa mafumbo;Na umbo la BWANA yeye ataliona.Mbona basi ninyi hamkuogopaKumnenea mtumishi wangu, huyo Musa?