12 Kisha Musa akatuma kuwaita Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu; nao wakasema, Hatuji sisi;
13 je! Ni jambo dogo, wewe kutuleta kutoka nchi iliyojawa na maziwa na asali, ili kutuua jangwani, lakini pamoja na haya wajikuza mwenyewe uwe mkuu juu yetu kabisa?
14 Kisha, hukutuleta katika nchi iliyojawa na maziwa na asali, wala hukutupa urithi wa mashamba, na mashamba ya mizabibu; je! Unataka kuwatoboa macho watu hawa? Hatuji.
15 Musa akakasirika sana, akamwambia BWANA. Usiikubali sadaka yao; mimi sikutwaa hata punda mmoja kwao, wala sikumwumiza hata mtu mmoja miongoni mwao.
16 Kisha Musa akamwambia Kora, Wewe na mkutano wako wote iweni hapa mbele ya BWANA kesho, wewe, na wao, na Haruni;
17 mkatwae kila mtu chetezo chake, na kutia uvumba juu yake, mkavilete mbele za BWANA, vyetezo mia mbili na hamsini; wewe pia, na Haruni, kila mtu na awe na chetezo chake.
18 Basi wakavitwaa kila mtu chetezo chake, wakatia na moto ndani yake, wakatia na uvumba juu ya moto, na kusimama pale mlangoni pa hema ya kukutania, pamoja na Musa na Haruni.