35 Malaika wa BWANA akamwambia Balaamu Enenda pamoja na watu hawa, lakini neno lile nitakalokuambia, ndilo utakalosema. Basi Balaamu akaenda pamoja na wakuu wa Balaki.
36 Balaki aliposikia ya kuwa Balaamu amefika, akatoka kwenda kumlaki, mpaka Mji wa Moabu, ulioko katika mpaka wa Arnoni, ulioko katika upande wa mwisho wa mpaka huo.
37 Balaki akamwambia Balaamu, Je! Mimi sikutuma watu kwako kwa bidii ili kukuita? Mbona hukunijia? Je! Siwezi mimi kukufanyizia heshima nyingi?
38 Balaamu akamwambia Balaki, Tazama, nimekujia. Je! Mimi sasa nina uwezo wo wote kusema neno lo lote? Neno lile Mungu atakalolitia kinywani mwangu, ndilo nitakalolisema.
39 Balaamu akaenda pamoja na Balaki wakafika Kiriath-husothi.
40 Balaki akachinja ng’ombe, na kondoo, akampelekea Balaamu na wale wakuu waliokuwa pamoja naye.
41 Ikawa asubuhi Balaki akamchukua Balaamu, akampandisha hata mahali pa juu pa Baali; na kutoka huko akawaona watu, hata pande zao za mwisho.