9 Kisha watatwaa nguo ya rangi ya samawi, na kukifunika kinara cha taa ya nuru, na taa zake, na makasi yake, na sahani zake za kutilia makaa, na vyombo vyake vyote vya mafuta, watumiavyo kwa kazi yake;
10 nao watakitia, na vyombo vyake vyote, ndani ya ngozi ya pomboo, na kukitia juu ya miti ya kukichukulia
11 Tena watatandika nguo ya rangi ya samawi juu ya madhabahu ya dhahabu, na kuifunika kwa ngozi za pomboo, na kuitia ile miti yake;
12 kisha watavitwaa vile vyombo vyote vya utumishi wavitumiavyo katika mahali patakatifu, na kuvitia katika nguo ya rangi ya samawi, na kuvifunika kwa ngozi za pomboo, na kuvitia juu ya miti ya kuvichukulia.
13 Nao watayaondoa hayo majivu madhabahuni; na kutandika nguo ya rangi ya zambarau juu yake;
14 nao wataweka vyombo vyake vyote juu yake ambavyo wavitumia katika madhabahu, vyetezo, na nyuma, na miiko, na mabakuli, vyombo vyote vya hiyo madhabahu; nao watatandika juu yake ngozi za pomboo, na kutia miti yake mahali pake.
15 Na Haruni na wanawe watakapokwisha kupafunika mahali patakatifu, na vyombo vyote vya mahali patakatifu, hapo watakapong’oa kambi; baadaye, wana wa Kohathi watakuja kuvichukua; lakini wasiviguse vile vitu vitakatifu, wasife. Vyombo vile ni mzigo wa wana wa Kohathi katika hema ya kukutania.