21 Tazama, BWANA, Mungu wako, ameiweka nchi mbele yako; haya panda, itamalaki, kama BWANA, Mungu wa baba zako, alivyokuambia; usiogope wala usifadhaike.
22 Nanyi mkanikaribia kila mmoja wenu, mkasema, Na tupeleke watu mbele yetu, ili watupelelezee nchi na kutuletea habari za njia itupasayo kuipandia, na za miji tutakayoifikia.
23 Neno hili likanipendeza sana; nikatwaa watu kumi na wawili, mtu mmoja wa kila kabila.
24 Nao wakageuka, wakapanda mlimani wakafika bonde la Eshkoli, wakalipeleleza.
25 Wakatwaa baadhi ya matunda ya nchi ile mikononi mwao, wakatuletea huku chini, wakatuletea habari tena, wakasema, Nchi hii anayotupa BWANA, Mungu wetu, ni nchi njema.
26 Lakini hamkukubali kukwea huko, mlihalifu neno la BWANA, Mungu wenu;
27 mkanung’unika hemani mwenu, mkasema, Ni kwa sababu BWANA ametuchukia, ndipo akatutoa katika nchi ya Misri, apate kututia katika mikono ya Waamori, ili kutuangamiza.