23 ndipo BWANA atakapowafukuza mataifa haya yote mbele yenu, nanyi mtamiliki mataifa makubwa yenye nguvu kuwapita ninyi.
24 Kila mahali mtakapokanyaga kwa nyayo za miguu yenu patakuwa penu; tokea hilo jangwa, na Lebanoni, na tokea mto wa Frati, mpaka bahari ya magharibi, itakuwa ndiyo mipaka yenu.
25 Hapatakuwa na mtu atakayeweza kusimama mbele yenu; BWANA, Mungu wenu, ataweka utisho wenu na kuhofiwa kwenu juu ya nchi yote mtakayoikanyaga, kama alivyowaambia.
26 Angalieni, nawawekea mbele yenu hivi leo baraka na laana;
27 baraka ni hapo mtakapoyasikiza maagizo ya BWANA, Mungu wenu, niwaagizayo leo;
28 na laana ni hapo msiposikiza maagizo ya BWANA, Mungu wenu, mkikengeuka katika njia niwaagizayo leo, kwa kuandama miungu mingine msiyoijua.
29 Tena itakuwa, atakapokuleta BWANA, Mungu wako, na kukutia katika nchi uendeayo kuimiliki, ndipo uiweke baraka juu ya mlima wa Gerizimu, na laana uiweke juu ya mlima wa Ebali.