3 Itengeze njia, igawanye na mipaka ya nchi yako, akurithishayo BWANA, Mungu wako, iwe mafungu matatu, ili kwamba kila mwenye kuua mtu apate kukimbilia huko.
4 Na hii ndiyo hukumu ya mwenye kuua mtu, atakayekimbilia huko awe hai; atakayemwua mwenziwe pasipo kukusudia, wala hakumchukia tangu hapo;
5 kama aingiapo mtu na mwenziwe mwituni kwenda kukata kuni, akapeleka mkono wake na shoka ili kukata mti, likatoka shoka katika mpini, likampiga yule mwenziwe hata akafa; basi na akimbilie katika miji hii mmojawapo awe hai;
6 asije akaandamiwa mwuaji na mwenye kulipiza kisasi cha damu, moyo wake ukali na hasira, akampata kwa njia kuwa ndefu, akamwua; wala hana haki ya kuuawa, kwa kuwa hakumchukia tangu hapo.
7 Kwa sababu hii ninakuamuru, na kukuambia, Ujitengee miji mitatu.
8 Na kama BWANA, Mungu wako, akiueneza mpaka wako kama alivyowaapia baba zako, akakupa na nchi yote aliyoahidi kwamba atawapa baba zako;
9 nawe ukiyashika maagizo haya yote nikuagizayo leo, na kuyafanya, kumpenda BWANA, Mungu wako, na kwenda sikuzote katika njia zake, ndipo ujiongezee miji mitatu tena, pamoja na mitatu ile;