1 Utokapo kwenda vitani kupigana na adui zako, na kuona farasi, na magari, na watu wengi kuliko wewe, usiwaogope; kwa kuwa BWANA Mungu wako, yu pamoja nawe, aliyekukweza kutoka nchi ya Misri.
2 Na iwe, msongeapo mapiganoni, kuhani na akaribie na kusema na watu,
3 awaambie, Sikizeni, enyi Israeli, hivi leo mwasongea mapiganoni juu ya adui zenu mioyo yenu na isizime; msiche, wala msiteteme, wala msiingiwe na hofu kwa ajili ya wao;
4 kwa maana BWANA, Mungu wenu, ndiye awaandamaye kwenda kuwapigania juu ya adui zenu, ili kuwaokoa ninyi.
5 Na maakida na waseme na watu, na kuwaambia, Ni mtu gani aliye hapa aliyejenga nyumba mpya, wala hajaiweka wakfu? Aende akarudi nyumbani kwake, asije akafa mapiganoni, ikawekwa wakfu na mtu mwingine.