3 Na huyo mumewe wa sasa akimchukia, na kumwandikia hati ya kumwacha, na kumpa mkononi mwake, na kumtoa katika nyumba yake; au akifa yeye mumewe wa sasa, aliyemtwaa kuwa mkewe;
4 yule wa kwanza aliyemwacha asimtwae kuwa mkewe tena, akiisha kutiwa unajisi; kwa kuwa haya ni machukizo mbele za BWANA; kwa hiyo usiitie dhambini nchi, akupayo BWANA, Mungu wako, iwe urithi.
5 Mtu atwaapo mke mpya, asiende vitani pamoja na jeshi, wala asipewe shughuli juu yake yo yote; akae faragha mwaka mmoja nyumbani mwake, apate mfurahisha mkewe aliyemtwaa.
6 Mtu awaye yote asitwae jiwe la kusagia, la juu wala la chini, kuwa rehani; kwani hivi ni kutwaa maisha ya mtu kuwa rehani.
7 Mtu akionekana anamwiba nduguze mmojawapo katika wana wa Israeli, akamfanya kama mtumwa, au kumwuza; na afe mwivi huyo; ndivyo utakavyoondoa uovu katikati yako.
8 Angalia katika pigo la ukoma, utunze kwa bidii, kwa kufanya mfano wa yote watakayowafundisha makuhani Walawi; tunzeni kwa kuyafanya vile vile kama nilivyowaamuru wao.
9 Kumbukeni na BWANA, Mungu wako alivyomtenda Miriamu katika njia mlipotoka Misri.