10 Na mataifa yote ya duniani watakuona umeitwa kwa jina la BWANA, nao watakuwa na hofu kwako.
11 BWANA atakufanya uwe na wingi wa uheri, katika uzao wa tumbo lako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, na uzao wa nchi yako, katika nchi BWANA aliyowaapia baba zako kwamba atakupa.
12 Atakufunulia BWANA hazina yake nzuri, nayo ni mbingu, kwa kutoa mvua ya nchi yako kwa wakati wake, na kwa kubarikia kazi yote ya mkono wako; nawe utakopesha mataifa mengi, wala hutakopa wewe.
13 BWANA atakufanya kuwa kichwa, wala si mkia; nawe utakuwa juu tu, wala huwi chini; utakapoyasikiza maagizo ya BWANA, Mungu wako, nikuagizayo hivi leo, kuyaangalia na kufanya;
14 msipokengeuka katika maneno niwaamuruyo leo kwa lo lote, kwenda mkono wa kuume wala wa kushoto, kwa kuifuata miungu mingine na kuitumikia.
15 Lakini itakuwa usipotaka kuisikiza sauti ya BWANA, Mungu wako, usiyaangalie kufanya maagizo yake yote na amri zake, nikuagizazo hivi leo, ndipo zitakapokujia laana hizi zote na kukupata.
16 Utalaaniwa mjini, utalaaniwa na mashambani.