12 ili uingie katika agano la BWANA, Mungu wako, na kiapo chake, afanyacho nawe BWANA, Mungu wako, hivi leo;
13 apate kukuweka leo uwe taifa kwake naye apate kuwa Mungu kwako, kama alivyokuambia, na kama alivyowaapia baba zako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo.
14 Wala sifanyi na ninyi peke yenu agano hili na kiapo hiki;
15 ila na yeye aliyesimama hapa nasi hivi leo mbele ya BWANA, Mungu wetu, na yeye naye asiyekuwapo pamoja nasi leo;
16 (kwani mwajua mlivyoketi nchi ya Misri, na tulivyo kuja katikati ya mataifa hayo mliyopita katikati yao;
17 nanyi mliona machukizo yao, na sanamu zao, miti na mawe, fedha na dhahabu, zilizokuwako kwao;)
18 asiwe mtu katikati yenu, mume wala mke, wala jamaa, wala kabila, ageukaye moyo wake leo amwache BWANA, Mungu wetu, kwenda kuitumikia miungu ya mataifa hayo; lisiwe katikati yenu shina lizaalo uchungu na pakanga;