18 asiwe mtu katikati yenu, mume wala mke, wala jamaa, wala kabila, ageukaye moyo wake leo amwache BWANA, Mungu wetu, kwenda kuitumikia miungu ya mataifa hayo; lisiwe katikati yenu shina lizaalo uchungu na pakanga;
19 ikawa asikiapo maneno ya laana hii, ajibarikie mtu huyo moyoni mwake, na kusema, Nitakuwa katika amani, nijapotembea katika upotoe wa moyo wangu kwa kuangamiza mbichi na kavu;
20 BWANA hatamsamehe mtu huyo, lakini wakati huo hasira ya BWANA na wivu wake vitafuka moshi juu ya mtu yule, na laana yote iliyoandikwa katika kitabu hiki itamkalia juu yake, na BWANA atalifuta jina lake chini ya mbingu.
21 BWANA atamtenga kwa uovu, kutoka kabila zote za Israeli, kwa laana zote za agano lililoandikwa katika chuo hiki cha torati.
22 Na kizazi cha baadaye, wanenu watakaoinuka baada yenu, na mgeni atakayekuja kutoka nchi ya mbali, watasema, watakapoyaona mapigo ya nchi ile, na magonjwa aliyoitia BWANA;
23 ya kuwa nchi yake nzima ni kibiriti, na chumvi, na kuteketea, haipandwi, wala haizai, wala nyasi hazimei humo, kama mapinduko ya Sodoma na Gomora, Adma na Seboimu, aliyoipindua BWANA kwa ghadhabu yake na hasira zake;
24 mataifa yote watasema, Mbona BWANA ameifanyia hivi nchi hii? Ni nini maana yake hari ya hasira hizi kubwa?