14 BWANA akaniamuru wakati ule niwafundishe maagizo na hukumu, mpate kuzitenda katika nchi ile mtakayoivukia ili kuimiliki.
15 Jihadharini nafsi zenu basi; maana hamkuona umbo la namna yo yote siku ile BWANA aliyosema nanyi kutoka kati ya moto;
16 msije mkajiharibu nafsi zenu, mkajifanyia sanamu ya kuchonga, mfano wa sura yo yote, mfano wa mwanamume au mwanamke,
17 mfano wa mnyama ye yote aliye duniani, au mfano wa ndege ye yote arukaye mbinguni,
18 au mfano wa kitu cho chote kitambaacho juu ya ardhi, au mfano wa samaki ye yote aliye majini chini ya nchi;
19 tena usije ukainua macho yako hata mbinguni, na ulionapo jua, na mwezi, na nyota, jeshi la mbinguni lote pia, ukashawishwa na kuviabudu, na kuvitumikia, ambavyo BWANA, Mungu wako amewagawanyia watu wote chini ya mbingu zote.
20 Bali BWANA amewatwaa ninyi, na kuwatoa katika tanuu ya chuma, katika Misri, mpate kuwa watu wa urithi kwake, kama mlivyo leo hivi.