3 Basi jua siku hii ya leo kuwa BWANA, Mungu wako, ndiye atanguliaye kuvuka mbele yako kama moto uteketezao; atawaangamiza, tena atawaangusha mbele yako; ndivyo utakavyowafukuza na kuwapoteza upesi, kama alivyokuambia BWANA.
4 Usiseme moyoni mwako, BWANA, Mungu wako, atakapokwisha kuwasukumia nje mbele yako, ukasema, Ni kwa haki yangu alivyonitia BWANA niimiliki nchi hii; kwani ni kwa ajili ya uovu wa mataifa haya BWANA awafukuza nje mbele yako.
5 Si kwa haki yako, wala kwa unyofu wa moyo wako, hivi uingiavyo kuimiliki nchi yao; lakini ni kwa uovu wa mataifa haya BWANA, Mungu wako, awafukuza nje mbele yako; tena apate kuliweka imara hilo neno BWANA alilowaapia baba zako Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo.
6 Basi jua ya kuwa BWANA, Mungu wako, hakupi nchi hii nzuri uimiliki kwa ajili ya haki yako, kwa maana u taifa lenye shingo ngumu.
7 Kumbuka, usisahau ulivyomtia BWANA, Mungu wako, kasirani jangwani; tangu siku uliyotoka nchi ya Misri hata mlipofika mahali hapa, mmekuwa na uasi juu ya BWANA
8 Tena mlimkasirisha BWANA katika Horebu, BWANA akakasirika nanyi hata akataka kuwaangamiza.
9 Na hapo nilipokwea mlimani kwenda kuzipokea mbao za mawe, nazo ni mbao za agano BWANA alilofanya nanyi, ndipo nikakaa mle mlimani siku arobaini usiku na mchana; sikula chakula wala kunywa maji.