2 na Musa peke yake ndiye atakayekaribia karibu na BWANA; lakini hao hawatakaribia karibu; wala hao watu hawatakwea pamoja naye.
3 Musa akaenda akawaambia watu maneno yote ya BWANA, na hukumu zake zote; watu wote wakajibu kwa sauti moja, wakasema, Maneno yote aliyoyanena BWANA tutayatenda.
4 Basi Musa akayaandika maneno yote ya BWANA, akaondoka asubuhi na mapema, akajenga madhabahu chini ya mlima, na nguzo kumi na mbili, kwa hesabu ya kabila kumi na mbili za Israeli,
5 akapeleka vijana wa wana wa Israeli, waliotoa sadaka za kuteketezwa, wakamchinjia BWANA sadaka za amani za ng’ombe.
6 Musa akatwaa nusu ya ile damu, akaitia katika mabakuli; na nusu ya ile damu akainyunyiza juu ya madhabahu.
7 Kisha akakitwaa kitabu cha agano akakisoma masikioni mwa watu; wakasema, Hayo yote aliyoyanena BWANA tutayatenda, nasi tutatii.
8 Musa akaitwaa ile damu, akawanyunyizia watu, akasema, Hii ndiyo damu ya agano alilolifanya BWANA pamoja nanyi katika maneno haya yote.