46 Siku zote ambazo pigo li ndani yake, yeye atakuwa mwenye unajisi; yeye yu najisi; atakaa peke yake; makazi yake yatakuwa nje ya marago.
47 Tena, vazi nalo ambalo pigo la ukoma li ndani yake, kwamba ni vazi la sufu, au kwamba ni la kitani;
48 likiwa limefumwa, au kusokotwa; likiwa ni la kitani au la sufu; kwamba ni katika ngozi, au kitu cho chote kilichofanywa cha ngozi;
49 hilo pigo likiwa la rangi ya majani au jekundu, katika vazi, au katika ngozi, au katika lililofumwa, au katika lililosokotwa, au katika kitu cho chote cha ngozi; ni pigo la ukoma, nalo ataonyeshwa kuhani;
50 na kuhani ataliangalia hilo pigo, naye atakiweka mahali kile kilicho na pigo muda wa siku saba;
51 kisha siku ya saba ataliangalia hilo pigo; kama pigo limeenea katika hilo lililofumwa, au katika hilo lililosokotwa, au katika ngozi, ijapokuwa hiyo ngozi ina matumizi yo yote; hilo pigo ni ukoma unaokula; vazi hilo ni najisi.
52 Naye atalichoma moto vazi hilo, kwamba ni lililofumwa au kwamba ni lililosokotwa, kama ni la sufu, au la kitani, au kitu cho chote cha ngozi, ambacho kina hilo pigo ndani yake; kwa maana, ni ukoma unaokula; vazi hilo litachomwa moto;