1 BWANA akamwambia Musa, akisema,
2 Sema na Haruni, na wanawe, na wana wote wa Israeli, ukawaambie; Neno hili ndilo aliloliamuru BWANA, akisema,
3 Mtu awaye yote wa nyumba ya Israeli atakayechinja ng’ombe, au mwana-kondoo, au mbuzi, ndani ya marago, au atakayemchinja nje ya marago,
4 wala hamleti mlangoni pa hema ya kukutania, ili amtoe kuwa matoleo kwa BWANA mbele ya hema ya BWANA; mtu huyo atahesabiwa kuwa ana hatia ya damu; amemwaga damu; na mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake;
5 ili kusudi wana wa Israeli walete sadaka zao, wazichinjazo mashambani, naam, wazilete kwa BWANA, mpaka mlango wa hema ya kukutania, kwa huyo kuhani, ili wazichinje ziwe sadaka za amani kwa BWANA.
6 Naye kuhani atainyunyiza damu yake juu ya madhabahu ya BWANA, mlangoni pa hema ya kukutania, na kuyateketeza mafuta yake, yawe harufu njema mbele za BWANA.
7 Wala hawatatoa tena sadaka zao kwa wale majini, ambao huwafuata ili wafanye uasherati nao. Sheria hii itakuwa sheria ya milele kwao, kizazi baada ya kizazi.