20 Tena mtu mume akilala na mke wa mjomba wake, ameufunua utupu wa mjomba wake; watauchukua uovu wao; watakufa bila kuzaa mwana.
21 Tena mtu mume akimtwaa mke wa nduguye, ni uchafu; ameufunua utupu wa nduguye; hao watakuwa hawana wana.
22 Basi zishikeni amri zangu zote, na hukumu zangu zote, na kuzifanya; ili kwamba hiyo nchi, ambayo nawapeleka ninyi kukaa, isiwatapike.
23 Nanyi msiende kwa kuziandama desturi za taifa, niitoayo mbele yenu; kwa kuwa wao waliyafanya mambo hayo yote, na kwa ajili ya hayo niliwachukia.
24 Lakini mimi nimewaambia ninyi, Mtairithi nchi yao, nami nitawapa ninyi kuimiliki; nchi iliyojaa maziwa na asali; mimi ni BWANA, Mungu wenu, niliyewatenga ninyi na mataifa.
25 Kwa ajili ya hayo mtapambanua kati ya mnyama aliye safi na mnyama aliye najisi, na kati ya ndege aliye tohara na ndege aliye najisi; nanyi msizifanye nafsi zenu kuwa machukizo kwa njia ya mnyama, au kwa njia ya ndege, au kwa njia ya kitu cho chote ambacho nchi imejaa nacho, niliowatenga nanyi kuwa ni najisi.
26 Nanyi mtakuwa watakatifu kwangu mimi; kwa kuwa mimi BWANA ni mtakatifu nami nimewatenga ninyi na mataifa, ili kwamba mwe wangu.