7 Jua likiisha kuchwa atakuwa safi; kisha baadaye atakula katika vitu vitakatifu, maana ni chakula chake.
8 Nyamafu au mnyama aliyeraruliwa na wanyama asile, asijitie unajisi kwa hiyo nyama; mimi ndimi BWANA.
9 Basi kwa hiyo watayashika mausia yangu, wasije wakachukua dhambi kwa hayo, nao wakafa humo, wakiyanajisi; mimi ndimi BWANA niwatakasaye.
10 Mgeni awaye yote asile katika kitu kitakatifu; mgeni wa kuhani akaaye kwake, au mtumishi aliyeajiriwa, asile katika kitu kitakatifu.
11 Lakini kwamba kuhani akinunua mtu ye yote, kwa kumnunua kwa fedha zake, yeye atakula katika hicho; na hao waliozaliwa nyumbani mwake watakula katika chakula chake.
12 Na binti ya kuhani kwamba ameolewa na mgeni, asile katika sadaka ya kuinuliwa katika vitu vile vitakatifu.
13 Lakini kwamba binti ya kuhani ni mjane, au kwamba ameachwa na mumewe, wala hana mtoto, kisha amerudi na kuketi katika nyumba ya baba yake, kama vile katika ujana wake, yeye atakula katika chakula cha baba yake; lakini mgeni awaye yote asile katika chakula hicho.